MAMBO HAYAJILETI YENYEWE – MAMBO YANASABABISHWA KUTOKEA!

“5Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu,katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa….(2Petro 1:5)
Bwana akufunulie akili zako ili uelewe hiki tunachojifunza lakini pia akusaidie kuyaweka kwenye matendo haya unayojifunza. Sasa hivi tunaishi kwenye nyakati ambazo kumezuka mafundisho yenye msisitizo mkubwa sana kwenye upande mmoja wa miujiza kiasi kwamba watu wengi sana wamejikuta wanaishi maisha ya kimiujiza miujiza,naamanisha watu wamekuwa wanaishi wakitegemea kufanikiwa katika maisha kwa miujiza tu unakuta mtu hataki kufanya kazi anategemea akienda kuwekewa mikono na watumishi basi mambo yatajileta yenyewe tu! Kwa sababu ya watu wengi kutaka kuishi kimiujiza wamejikuta kila kitu wanaita muujiza, unakuta mtu kafanikiwa kununua gari eti anaita muujiza au mtu kwenda ulaya anaita muujiza, mama kanunuliwa kanga na mumewe anaita muujiza. Sijui kwa nini nimeanza kwa style hii lakini ninamini kuna kitu Mungu anataka tujifunze hapa na nianze kuelezea kuhusu muujiza. Ukisoma katika kamusi ya Kiswahili sanifu inafafanua neno muujiza kama jambo lisilokuwa la kawaida. Kwa maana nyingine muujiza ni matendo yanayofanyika kinyume na maumbile ya asili ni mambo ambayo hata ukimwambia mwanasayansi afafanue hawezi kuyafafanua yametokeaje, lakini utakuta mtumishi wa Mungu anamuombea mtu anasema ,”pokea muujiza wa kwenda ulaya! Pokea muujiza wa gari pokea muujiza wa nyumba! Na maombi mengine mengi ambayo ninaamini msomaji unayafahamu au umeshawahi kuombewa. Nisikilize nikwambie kama hayo maombi unayoombewa yangekuwa yanatokea, mfano unaambiwa pokea muujiza wa gari halafu gari inatokea from no where au ukienda nyumbani unaikuta gari imepark hujui ilikotoka haina mwenyewe basi huo ndo muujiza lakini ukichukua hela ukaenda mwenyewe kununua gari hapo kuna muujiza gani ndugu? Au unaombewa pokea muujiza wa kwenda ulaya halafu ghafla unajikuta uko ulaya hujui umefikaje huo nao ni muujiza. Kitu gani nataka ujifunze hapa? Uache kuishi maisha ya kimiujiza kwa sababu mambo hayajileti yenyewe yanasababishwa kutokea,utanielewa tu huko mbele! Angalia Biblia yako nikuonyeshe mifano michache kuhusu miujiza halafu tuendelee, kutoka 7:10-12 inasema,
“10………Haruni akabwaga fimbo yake chini mbele ya farao,mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka.
11Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi;na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo Kwa uganga wao. 12Wakabwaga kila mtu fimbo yake,nazo zikawa nyoka;lakini fimbo ya Haruni Ikazimeza fimbo zao”.
Sikia! hata ungewaita wanasayansi hapo hakuna ambaye angekueleza ile fimbo ya Musa na za wachawi ziligeuka vipi zikawa nyoka! Huo ulikuwa muujiza lakini nataka ujifunze mambo machache hapa, kwanza fahamu Mungu anatenda miujiza lakini pia kama hufahamu shetani naye anatenda miujiza! Umeona hapo fimbo ya Musa ilipotupwa chini iligeuka nyoka na wachawi wa farao wakatupa zao nazo zikawa nyoka lakini (naupenda sana huu mstari) fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zile za wachawi! Unajua maana yake? Ni hivi, kile kitendo cha fimbo ya Haruni kumeza fimbo za wachawi Mungu alikuwa anamaanisha kwamba yeye ni mkubwa kuliko shetani,alikuwa anamaanisha muujiza wake ni mkubwa na unadumu kuliko wa shetani!
Ngoja niishie hapo Mungu akitoa nafasi nitakuja na somo linalohusiana na miujiza na Baraka maana hivi ni vitu vinavyowasumbua sana watu kiasi cha kuwafanya waishi maisha ya kutanga tanga kwa kuhama kanisa hili kwenda kanisa jingine. Sasa angalia maneno anayosema Mtume Petro wakati analiandikia kanisa waraka wake wa kwanza na ninachotaka uone hapo ni yale maneno anayosema “mkijitahidi kwa UPANDE WENU”! Sijui kama umeshawahi kutafakari mstari huu kwa makini na ukangundua yaliyojificha hapo; Petro anaposema kwa upande wenu ina maanisha kuna sehemu yako wewe kufanya kwa upande wako na kama kuna upande wako kufanya kitu basi pia kuna sehemu ya Mungu kufanya kwa upande wake na ndio maana kichwa cha somo kinasema mambo hayajileti yenyewe kwa sababu kuna kitu unatakiwa kufanya kwa upande wako ambapo ukikiunganisha na upande anaofanya Mungu unapata jibu lako! Ngoja twende na mifano, angalia yeremia 29:12 – 14 inasema hivi:-
12 Nanyi mtaniita,mtakwenda na kuniomba,nami nitawasikiliza.13 Nanyi mtanitafuta,na kuniona,mtakaponitafuta Kwa moyo wenu wote.14 Nami nitaonekana,asema BWANA,nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa……………….”.
Kwa tafsiri rahisi ni kama Mungu anasema,kwa upande wenu mnachotakiwa kufanya ni kuniita,mnachotakiwa kufanya ni kuniomba na kwa upande wangu ninachotakiwa ni kuwasikiliza,na kujionyesha kwenu! Maana yake ni nini? Kama huiti Mungu hawezi kuitika! Ndiyo! Ataitikaje wakati hajaitwa? Mpendwa unakumbuka ule mstari ambao hata ukimuuliza mtu asiye na tabia ya kusoma biblia atakutajia mstari huo? Ni ule wa mathayo 7:7, hebu uangalie kwa namna hii nilivyofanya ili kukurahisishia kuelewa!
Upande wako kufanya kitu upande wa Mungu kufanya kitu
Ombeni nanyi (kuomba) mtapewa (kukupa unachoomba)
Tafuteni nanyi (kutafuta) mtaona (kukuonyesha unachotafuta)
Bisheni nanyi (kubisha/kupiga hodi) mtafunguliwa (kukufungulia malango)

Kumbuka mambo hayajileti yenyewe bali yanasababishwa kutokea na kwasababu hiyo hauwezi kufanikiwa katika jambo lolote kama utakuwa ni mtu wa kukaa na kusubiri Mungu afanye kitu na hata kama Mungu akifanya kitu amefanya kwa upande wake kama wewe hujafanya kwa upande wako hauwezi kupata matokeo! Angalia mfano huu nikuonyeshe kitu, fungua Yohana 9:6-7 inasema hivi,
“6 Alipokwisha kusema hayo,alitema mate chini,akafanya tope kwa yale mate.
Akampaka kipofu tope za macho,7 akamwambia,nenda kanawe katika birika ya Siloamu,
(maana yake aliyetumwa).Basi akaenda na kunawa;akarudi anaona”.
Hii ni habari ya mtu mmoja aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa na kwa bahati akakutana na Yesu lakini katika kuponywa kwake kuna kitu alitakiwa afanye kwa upande wake ili kukamilisha uponyaji wake na kilikuwa ni kwenda kunawa kwenye birika ya siloamu na biblia inasema akaenda na kunawa akarudi anaona! Kama yule kipofu angeamua kudharau akapitiliza na kuendelea na mambo yake mengine asiende kunawa ninakwambia angebaki kipofu hivyo hivyo lakini si kwa sababu Mungu hakufanya kitu,hapana, Mungu alishafanya kwa upande wake na ilibaki sehemu yake yule kipofu kufanaya ili kukamilisha uponyaji wake!
Okey! Angalia mfano wa mtu mmoja aliyekuwa na ukoma jina lake Naamani, huyu alimwendea mtumishi wa Mungu Elisha baada ya kusikia kuwa anaweza kumponya. Alipofika kwa Elisha,alitumiwa ujumbe wa mtu kumwambia kuwa aende katika mto Yordani akajichovye mara saba na ngozi ya mwili wake itarudi kuwa kawaida kabisa. Naamani aliposikia hivyo alikasirika na kusema,”Tazama,nilidhania,bila shaka atatoka kwangu, na kusimama na kuomba kwa jina la BWANA,Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je abana na farpari,mito ya Dameski si bora kuliko mito yote ya Israel? Siwezi kujiosha ndani yake na kuwa safi? Akageuka akaondoka kwa hasira”.
(soma habari hii katika kitabu cha 2wafalme 5:9-14) Haya ndiyo mwazo waliyonayo watu wengi sana wanapokwenda kanisani au kwenye semina na mikutano ya neno la Mungu au wanapofanyiwa maombezi. Unakuta mtu haamini mpaka awekewe mikono na mtumishi, lakini nataka nikwambie kitu kimoja ambacho watu wengi wamekuwa wanakosea ambacho ni kutokuafuata maagizo wanayopewa na watumishi au kutofuata vile neno linavyosema. Sikia! Kama umeambiwa kanawe katika birika ya siloamu nenda kanawe! Kama umeambiwa kajioshe kwenye mto yordani, nenda kajioshe! Kama umeambiwa endelea mbele hata kama mbele yako kuna bahari, wewe endelea mbele!!! JUST DO IT! Upande wa Naamani ulikuwa ni kujiosha kwenye mto Yordani tu na hakuna kingine na ndio maana wale watumishi walimwambia maneno haya,”Baba yangu kama yule nabii angelikuambia kutenda jambo kubwa,usingalilitenda? Je si zaidi basi akikuambia,Jioshe uwe safi?” nachotaka kukuambia hapa ni wewe kufuata maagizo ya neno la Mungu linavyosema. Kwa hiyo nabii Elisha alifanya kwa upande wake na ulibakia upande wa muhitaji ambaye ni naamani, na lipokubalikufuata maagizo alipona kabisa!(haleluya!) Petro anasema mkijitahidi kwa upande wenu, (kumbuka hilo). Uko upande wako ambao unatakiwa kufanya kitu, sasa kwa sababu ya kutoelewa hili watu wamehangaika huku na huku katika makanisa wakiombewa lakini hawaoni mafanikio na hii ni kwa sababu wanafikiri mambo yatajileta yenyewe tu baada ya kuwekewa mikono na watumishi! Umeshawahi kukutana na wanafunzi waliookoka? Fuatilia maendeleo yao na utakuta wengi maendeleo yao si mazuri sana au wengine ni mabaya kwa sababu wamekuwa wakiamini kuwa ile kuokoka tu ni tiketi ya kufaulu, na kwa sababu hiyo unakuta hataki kusoma, yeye na biblia na maombi tena ukifika wakati wa mitihani wanajifariji kwa kusema Mungu amesema tutakuwa kichwa wala si mikia!(hii ni ajabu kabisa). Huku ni kushindwa kucheza au kufanya kwa upande wako na mtokeo yake ni kufeli na kuanza kulaumu Mungu, sikia mwanafunzi unayesoma ujumbe huu,jitahidi kwa upande wako kusoma kwa bidii na upande wa Mungu ni kukufunulia akili zako uelewe unachosoma na ukielewa unachosoma mitihani inapokuja ni lazima, narudia tena ni lazima lile neno la kuwa kichwa litimie!( Amen?)
Kitu ni kilekile hata katika maisha ya kila siku tunayoishi, watu wamekuwa wakitaka kubarikiwa na Mungu bila ya kuwa na hata na vyombo vya kukingia Baraka hizo! Angalia kanuni alizotoa Mungu juu ya Baraka halafu linganisha na wewe unavyoenda ni sawa? Fungua kumbukumbu la torati 28:1-8 inasema:-
“1 Itakuwa(shika hilo neno) utakapoisikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo,ndipo BWANA, Mungu wako atakapokutukuza juu ya mataifa yote duniani; 2 na Baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako. 3 utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. 4 utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako,na uzao wa wanyama wako wa mifugo,maongeo ya ng’ombe wako,na wadogo wa kondoo zako. 5 litabarikiwa KAPU lako, na CHOMBO chako cha kukandia unga…………..8 BWANA ataiamuru Baraka ije juu yako katika GHALA zako, na mambo yote unayotia mkono; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA Mungu wako.”
Hapo juu nimekuandikia kwenye mabano shika hilo neno nikimaanisha lile neno “itakuwa”. Itakuwa nini? Itakuwa Baraka za Mungu zitakujilia utakapoiskia sauti ya BWANA Mungu wako kwa bidii………………..! Siyo utakapowekewa mikono na kuombewa maombi ya kupokea muujiza wa kwenda ulaya au utakapowekewa mikono na kuombewa maombi ya kupokea muujiza wa gari, hapana! Bali itakuwa utakapoiskiliza sauti ya BWANA Mungu wako kwa bidii! Huo ni upande wako wewe kufanya kitu na upande wa Mungu ni kuiamuru Baraka ije juu yako lakini angalia kwa makini hiyo mistari ambayo nimeamua kuiandika kwa urefu badala ya kukupa kazi ya kwenda kusoma biblia na ninajua wengi ni wavivu kusoma biblia ndio maana napenda sana ninapoandika masomo yangu mistari yote niwe naiandika kama ilivyoandikwa kwenye biblia. Sasa Baraka ya Mungu inapoachiliwa juu yako itategemea na chombo ulicho nacho kwa ajili ya kukingia Baraka, pale juu nimeandika kuwa watu wengi wanataka kubarikiwa na Mungu lakini wakati huo huo hawana vyombo kwa ajili ya kukingia Baraka. Sikiliza! Wakati mwingine hupokei Baraka za Mungu si kwasababu umekosea au shetani amezuia bali ni kwa sababu huna chombo cha kukingia Baraka za Mungu zinapoachiliwa! Sijakosea, nasema hivi wakati mwingine hupokei Baraka za Mungu si kwa sababu umekosea au shetani amezuia bali ni kwa sababu huna chombo cha kukingia Baraka za Mungu zinapoachiliwa! Ngoja nikuulize swali hili, unaelewa nini pale biblia inaposema litabarikiwa KAPU lako? Au inaposema na CHOMBO chako cha kuakandia unga? Au anaposema utabarikiwa mjini utabarikiwa na mashambani? Au unafikiri Mungu aliposema utabarikiwa mjini ni kwa kuwa unazurura mjini au kukaa kwenye vijiwe vya kahawa na kuongelea habari za siasa tangu asubuhi hata jioni? Hii ikusaidie uamke sasa tunapokwenda kufunuliwa hiki na Bwana Yesu. Sasa unisikilize nikwambie! Kazi uliyo nayo ni kapu la kukingia Baraka za Mungu, duka ulilo nalo ni kapu la kukingia Baraka za mungu biashara uliyo nayo (nazungumzia biashara halali) ni kapu la kukingia Baraka za Mungu na kama ulikuwa hujui hata kipaji ulichonacho kiwe ni cha kucheza mpira au kuchekesha au kuimba au kukimbia au basket ball au kucheza tenis au kuigiza au kuchora ni kapu la kukingia Baraka za Mungu! Itakuwa utakapoisikiliza sauti ya Bwana Mungu wako kwa bidii Baraka zitamiminwa kwenye kapu lako haijalishi uko mjini au shambani, oooh! Itakuwa! Akiimimina kweye duka wateja watajaa (si lazima uende kwa waganga ndo duka lako lijae wateja)! Akiimimina kwenye kazi unayofanya mshahara lazima uongezwe pamoja na cheo! Akiimimina kwenye kapu lako la football kama wewe ni kipa magoli hayaingii hovyohovyo na kama wewe ni mshambuliaji hakuna beki atasimama mbele yako, kama ni beki hakuna mshambuliaji atapita kwako nafasi yoyote utang’aa tu! (sema amen!) akiimimina shambani hata kama mvua zitakuwa kidogo utavuna wakati wengine wakishangaa( soma habari ya Isaka utaelewa ninachosema)! Hapa niongee na wale mnaokimbilia mijini mkifikiri ndo kuna Baraka, inawezekana kabisa Mungu alikuwa anataka akubariki ukiwa shambani lakini wewe umekimbilia mjini na huko mambo yako ni magumu unaishi kimiujiza-miujiza lakini bado unajipa moyo kwa kusema kuishi mjini tu ni form six, hebu kaa na hiyo form six yako ya town na uone kama itakusaidia! Wewe umeacha kapu lako shambani umekimbilia mjini,halafu unata Mungu akubariki,sasa hata akijaza Baraka kwenye kapu lako utajuaje wakati kapu umeacha shambani? Jipange! Akiimimina kwenye mifugo ……..kasome habari ya Yakobo alipokwenda kuchunga mifugo ya mjomba wake Labani utaona nini kilitokea! Akiimimina kwenye kapu la kuigiza unapata kibali na kazi zako zinapendwa na unaanza kutengeneza hela kupitia kapu hilo la kuigiza! Ningeweza kusema mengi hapo lakini nataka nikuulize swali wewe unayesoma ujumbe huu, unataka Mungu akubarki ni sawa lakini unalo kapu la kukingia Baraka za Mungu zitakapomiminwa? Wengine wameacha makapu yao mashambani wamekimbilia mjini, aisee ninakwambia mambo hayajileti yenyewe bali yanasababishwa kutokea! Ni lazima ufanye kwa upande wako ili kuleta matokeo ya kile unachotaka kutoka kwa Mungu! Kumbuka Mtume Petro anasema,”Mkijitahidi kwa upande wenu”. Tulia kidogo utafakari kabla hatujaenda hatua nyingine, mwambie Mungu akusaidie ili tuweze kwenda sambamba na tukimaliza hapa usiwe kama ulivyokuwa!
Umemaliza kutafakari? Haya tuendelee, fungua kitabu cha 2falme 4:1-7 biblia inasema hivi:-
“1 Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema,Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha BWANA; na aliyemwia Amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa. 2 Elisha akamwambia,nikufanyie nini? Niambie una kitu gani nyumbani? Akasema mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani ila chupa ya mafuta. 3 Akasema, Nenda, ukatake VYOMBO huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu;
wala usitake vichache. 4 Kisha uingie ndani,ujifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. 5 Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina. 6 Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma. 7 Ndipo akaja akamwambia mtu wa Mungu, Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako” .
Hii ni habari inayomuhusu mama mjane aliyekuwa anadaiwa na kutokana na yeye kushindwa kulipa deni ilitakiwa awatoe watoto wake waende kutumikia deni hilo mpaka litakapokwisha. Lakini mama huyu hakuwa anataka watoto wake wakawe watumwa, kama ningekuwa nakufundisha kuhusu mwanamke jasiri basi pengine huu ungekuwa ni mojawapo ya mistari ambayo ningeitumia kwa kuwa huyu mama aliamua kupigana ili watoto wake wasijekwenda utumwani kwa sababu ya deni! Mama huyu alimwendea nabii Elisha na kumwambia shida yake lakini sikiliza Elisha anamjibu nini huyu mama, unajua anamwambia nikufanyie nini? Niambie unakitu gani nyumbani? Elisha kwa upande wake alikuwa na kitu ambacho anataka kumfanyia yule mama lakini kitu kile hakiwezi kukamilika mpaka kuna kitu yule mama amefanya kwa upande wake! Kumbuka hapo nyuma nimekwambia mambo hayajileti yenyewe, mambo yanasababishwa kutokea na Mtume Petro anasema mkijitahidi kwa upande wenu….!
Nataka nikufundishe mambo machache hapa na jambo la kwanza ni hili:-
1: Matatizo hayatatuliwi kwa wewe kuendelea kukaa kwenye tatizo na kulalamika juu ya hilo tatizo! Kama yule mama angekaa tu nyumbani pasipo kutafuta msaada alikuwa anawapoteza watoto wake kwa kuwa hakukuwa na jinsi yoyote ile wasiende utumwani! Kwa hiyo ni lazima uchukuke hatua badala ya kukaa kwenye tatizo na kulalamika. 2: Angalia mistari hii kutoka Luka 8:18 inasema, 18 Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye Kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile kitu ambacho anadhaniwa kuwa nacho”.
Sasa rudi kwenye maswali ambayo Elisha alimuuliza yule mama na angalia lile swali la pili alilomuuliza,alimuuliza hivi, “niambie una KITU (shika hilo neno)gani nyumbani? Sikiliza! Ili Mungu aweze kukutumia au kukusaidia ni lazima uwe na kitu ambacho kitamvuta Mungu kukutumia au kukusaidia! (tupo pamoja?) kasome biblia yako utaona hiki nachosema, wakati Mungu anamuita Musa alimkuta na fimbo alipomuuliza umeshika nini mkononi mwako Musa alisema fimbo, akamwambia itupe chini na alipoitupa ikageuka nyoka Musa akaogopa lakini Mungu akamwambia mshike mkiani, akamshika ikawa fimbo na tangu siku hiyo ile fimbo ikaitwa fimbo ya Mungu na miujiza mingi sana ilifanywa na Mungu kupitia ile fimbo! Siyo hicho tu kabla ya hapo Musa aliwahi kuua mmisri aliyekuwa anagombana na muisrael na hii ilikuwa sababu iliyomfanya akimbie misri na kwenda kuishi midiani, ndani mwake alikuwa na kitu cha tofauti cha kiuongozi na kiutumishi, hiki ndo Mungu alikiona ndani yake ila Musa alikitumia vibaya kwa kuua akifikiri ndo atakuwa amewasaidia waisrael. Wewe una kitu gani? Mungu anataka kukitumia hicho kitu kukusaidia au kukitumia katika kazi yake na ndo maana Elisha alimuuliza yule mama, una kitu gani nyumbani? Unamkumbuka Saul ambaye kabla ya kuitwa na Bwana alilitesa sana kanisa na kuwaua watumishi wa Mungu? Sikiliza! Kilichokuwa kinamsumbua Paul hata kufikia hatua ya kuwatesa watumishi wa Mungu kilikuwa ni wito na yeye alikuwa anajua kwa kufanya hivyo(kukamata watumishi na kuwaua au kuwaweka vifungoni) anamtumikia Mungu, na Mungu alikiona kitu kilichokuwa ndani ya Paul akaamua kumgeuza na kumtumia katika kazi yake! Kama unabisha rudi kwenye biblia kaangalie kazi aliyofaya Paul utakubaliana na mimi.Sasa wewe jaribu kusumbua watu wa Mungu na kuwaudhi wakati unajua kabisa unafanya makusudi na kwa chuki zako binafsi uone Mungu atakufanya nini! Angalia wito wa Daudi wengi sana hawajui nini kilimvutia Mungu kwa Daudi hata akamweka atawale watu wake Israeli. Daudi alikuwa na moyo wa tofauti na wakati akichunga kondoo wa baba yake huko porini alitokea simba akataka kula kondoo, Daudi alipambana na simba akamwua vile vile wakati mwingine alitokea dubu akataka kula kondoo lakini Daudi alipambana naye na kumuua. Sasa nisikilize! Kile alichofanya Daudi ndicho kitu kilichomvuta Mungu amtumie Daudi kuchunga watu wake maana Mungu aliangalia jinsi alivyojitoa kwa kondoo akajua huyu kama amefanya hivi kwa kondoo ambao ni wanyama atanifaa kwa ajili ya kondoo zangu(watu wake). Nenda katafute kwenye biblia yako kama kuna mahali Daudi aliwahi kushindwa vita au kama kuna mfalme katika Israel alikuwa mpiganaji kama Daudi! Biblia imesema katika mistari tuliyosoma hapo juu kwamba mwenye kitu atapewa na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile kitu ambacho anadhaniwa kuwa anacho. Ni hivi, kila mtu aliyeumbwa na Mungu ana KITU amabacho Mungu amempa ambacho kwa hicho Mungu atakitumia kupitishia Baraka zake katika maisha yake na katika kazi yake, sasa hicho kitu ukikitumia unaongezewa na kama hujakitumia kwa kujua au kutokujua utanyag’anywa! Ngoja nikwambie kitu kingine naona Napata mstari mwingine hapa,hebu angalia maneno haya kutoka kitabu cha 1Falme 17:12-16. Yanasema hivi, “12 Naye akasema,kama BWANA, Mungu wako aishivyo,sina mkate ila konzi ya unga katika pipa,na mafuta kidogo katika chupa;nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu,tuule tukafe. 13Eliya akamwambia,usiogope;enenda ukafanye kama ulivyosema;lakini unifanyie kwanza mkate mdogo uniletee;kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. 14 kwa kuwa BWANA,Mungu wa Israel,asema hivi,lile pipa la unga halitapunguka wala ile chupa ya mafuta haitaisha hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi. 15 Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya;na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. 16 Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa kinywa cha Eliya”.
Huu ni wakati ambao nabii Eliya alitangaza kutokuwepo kwa mvua kwa kipindi cha miaka mitatu na miezi sita na katika kipindi hicho kulikuwa na njaa ya kutisha na Mungu alimwambia Eliya aende akajifiche karibu na kijito cha kerithi na akawatuma kunguru wamlishe kwa kipindi mpaka kijito kile kilipokauka. Baada ya kukauka kwa kijito kile Mungu akamwambia Eliya aende katika nyumba ya mjane mmoja aliyeishi Sarepta. Eliya akafika kwa mama yule na akamkuta nje ya lango akiokota kuni; akamwambia, niletee maji na alipokuwa anakwenda kumletea maji akamwambia nakuomba uniletee kipande cha mkate mkononi mwako na hapa unaona akimjibu maneno tuliyosoma hapo juu. Sasa mimi sifundishi habari ya utoaji hapa ila nachotaka uone hapo ni kitu kile ambacho nimekuwa ninakufundisha hapo nyuma, kwamba ni lazima uwe na kitu ambacho Mungu akija kwako atakitumia kupitishia baraka zake kwa ajili yako na kwa ajili ya kazi yake. Yule mama alikuwa na konzi moja ya unga ambayo ilitosha kwa mlo mmoja tu wa yeye na mwanaye pamoja na mafuta kidogo kwenye chupa ambayo yangetosha kutumika kupikia mkate ule na matumini yao yalikuwa baada ya mlo ule wangesubiri kufa tu maana hawakuwa na jinsi nyingine ya kuishi. Lakini hakujua anyezungumza naye amekuja na nini, ooooh! Alikuwa amekuja na Baraka zisizokwisha, zilikuwa zinatafuta mtu mwenye kitu na kwa kutumia kile alichokuwa nacho yule mama yaani konzi moja ya unga na mafuta kidogo kwenye chupa Baraka zikamiminika kwenye ile nyumba ya mama mjane! Hapakuwa na njaa kwenye ile nyumba mpaka mvua iliponyesha maana pipa la unga lilikuwa haliishi unga wala chupa ya mafuta haikwisha! Unga ukiisha kwenye pipa Mungu anajaza mafuta yakiisha kwenye chupa Mungu anajaza! Ndiyo!! Kama vyombo vya kukingia Baraka vipo,Baraka zinamiminika tu wala hakuna mtu wa kuzuia! Wewe jipange tu! Ni kitu gani nataka uone hapo? Ni hiki, “mwenye kitu atapewa; na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile anadhaniwa kuwa nacho”.
Ngoja nikuambie mifano ya huku duniani kwa kukujengea ufahamu zaidi. Ni hivi, kwa wale wanaofahamu jinsi ya kupata mkopo kutoka bank au taasisi zinazohusika na ukopeshaji wanafahamu kuwa huwezi kwenda kwenye taasisi hizi kuomba mkopo mpaka uwe na kitu ambacho kwa hicho hawa jamaa watakuamini na kukupatia mkopo. Inawezekana ikawa ni nyumba, gari,kiwanja au mdhamini ambaye ana KITU ambacho kitawafanya hawa jamaa wakuamini na kukupatia mkopo. Nafikiri utakuwa umeelewa nini maana ya huo mstari unaosema “Mwenye kitu atapewa;na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile anachodhaniwa kuwa nacho”Ndiyo maana matajiri wanaendelea kuwa matajiri na masikini wamebaki kuwa masikini! Sasa angalia nukuu hii ambayo inatoka kwa mmoja wa watu ninaowakubali kwa kazi zao nzuri na huyu si mwingine bali ni Charles Kimei ambae ni mkurugenzi wa moja ya benki zenye mafanikio makubwa hapa nchini,naizungumzia benki ya CRDB na hapa nitoe shukrani kwa mtandao wa GK (gospel kitaa) ambao ndo nimeipata nukuu hii ambayo ndugu kimei aliitoa wakati wa misa ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Askofu wa dayosisi ya kaskazini ndugu Thomas Laizer. Kwa mujibu wa mtandao huo wa GK ndugu Kimei alisema hivi,” Askofu Laizer alikuwa ni mmoja wa wale watu, ambao sifa mojawapo ambayo mimi niliipenda na nimeiadmire, na ambayo ndio ilikuwa inaongoza sana dayosisi hii ni ya kuthubutu.
Alipokutana na mimi mara ya kwanza aliniambia kwamba, unafikiri nitafanya nini ili tuweza kukuza, kwanza kukuza ajira kwenye mkoa wetu na kwenye dayosisi yangu, na pili niweze kupata kitega uchumi ambacho kitasaidia dayosisi hii iweze kuwasaidia watu ambao wanahitaji, na zaidi ya hapo iweze pia kutekeleza shughuli za kimissioni ya dayosisi.
Nikamwambia Baba Askofu una nini? akasema usiniulize nina nini, mi nakuuliza wewe, utaweza kutusaidia? Nikamwambia, “lakini, unafirikiri mtu ukiwa na milioni moja, anaweza kuomba bilioni kumi?” Akaniambia anaweza, nikafurahi sana, nikajua huyu ni mtu ambaye ana think big.(mwisho wa kunukuu)
Sasa rudi kwenye somo ninalokufundisha,ndugu Kimei anasema mojawapo ya sifa aliyokuwa nayo Askofu Laizer ambayo yeye(Kimei) alikuwa anaipenda ni ile tabia yake ya kuthubutu. Nataka nikuambie kwamba Mungu anapenda watu wanaothubutu,nitakuonyesha huko mbele habari ya Petro na utaelewa hapo anaposema kuthubutu. Lakini kitu kingine anasema alipokutana kwa mara ya kwanza na Baba Askofu na kisha Askofu alipomuuliza kuwa afanye nini kukuza ajira katika mkoa wake na katika dayosisi yake na pili aweze kupata kitega uchumi kitakachoweza kuwasaidia wahitaji na kusaidia huduma ya injili? Sasa angalia kitu ambacho ndugu Kimei alimjibu Askofu, anasema hivi,”Nikamwambia Baba Askofu UNA NINI? Linganisha jibu la ndugu Kimei na jibu la Nabii Elisha alilomjibu yule mama mjane aliyekuwa akihitaji msaada kwake(tumeshasoma mistari huko nyuma). Alimwambia yule mama hivi,” nikufanyie nini? Niambie una kitu gani nyumbani? Nimekwambia nakufundisha mifano rahisi ya huku duniani ili kukujengea ufahamu kuhusu hiki tunachojifunza. Kitu kingine anasema ,nikamwambia,”Lakini unafikiri mtu akiwa na milioni moja anaweza kuomba bilioni kumi?” kabla sijaeleza kwenye majibu ya Baba Askofu nataka tena utafakari hilo swali ambalo ndugu Kimei alimuuliza Baba Askofu.(rudia tena kutafakari,kwamba mtu akiwa na milioni moja anweza kuomba bilioni kumi?) unapata kitu hapo? Ni hivi, Yeyote mwenye KITU(milioni moja) atapewa………..(bilioni kumi)……..” (Mungu msaidie huyu tu aelewe hapa). Nasema hivi, ukiwa na chupa ya mafuta(milioni moja) halafu ukaitumia kumimina kwenye vyombo vingine vikajaa vyote utakuwa umetengeneza zaidi…….(bilioni kumi). Tukirudi kwenye majibu ya Askofu unaona akijibu swali la ndugu Kimei kwa kusema,”Anaweza”. Sasa mwisho ndugu Kimei baada ya kujibiwa na Baba askofu kwamba inawezekana mtu akiwa na milioni moja akaomba bilioni kumi,alisema,’ nikafurahi sana, nikajua huyu ni mtu ambaye ana think big.” Nini maana maana ya ku-think big? Ni kuona ufito wa mlozi ninamaanisha kuona vema! Mungu alimuuliza Yeremia unaona nini? Yerermia akajibu naona ufito wa mlozi. Mungu akasema umeona vema.(soma Yeremia1:11-12). Huku ndiko ku-think big. Mungu anafurahi sana kuona watu wake wana-think big! ku-think big ni kuona nchi ya ahadi wakati mbele kuna bahari! Ku-think big ni kuona nchi ya ahadi hata kama mbele yako kuna majitu! Niishie hapo angalia jambo la tatu,
3: Mwombe Mungu akufundishe kujua na kutumia kitu alichokiweka ndani mwako ili kikusaidie katika maisha yako lakini pia katika kazi yake (Mungu). Yule mama alikuwa na chupa ya mafuta lakini alikuwa hajui thamani yake mpaka alipokwenda kwa mtumishi wa Mungu na kusaidiwa. Muda wote alikuwa anaona ni kitu cha kawaida tu kisicho na thamani yoyote kumbe hakujua kuwa hicho ndicho kitakacho mkomboa. Kitu ni kilekile tukirudi kwa upande wako unayesoma ujumbe huu, una chupa ya mafuta (kipaji) lakini aidha hujui thamani yake au hujui kuitumia ili ikusaidie katika maisha yako! Ujumbe huu umekuja kwa makusudi ya kukufahamisha na kukusaidia ili uweze kujua!
4: Ukijua kitu ulichonacho na ukajua kukitumia kinachofuata ni Baraka kumiminika kupitia hicho kitu. Sasa angalia kilichotokea kwa yule mama, Baraka zilikuwa zinataka vyombo ili zimiminike humo lakini mama hakuwa navyo akaenda kuazima kwa majirani na pamoja na kukusanya vyombo vingi(maana aliambiwa asitake vichache) bado Baraka zilikuwa ni nyingi kuliko vyombo alivyokusanya, maandiko yanasema vyombo vilipokwisha mafuta (baraka) yakakoma! Unajua maana yake? Ukiwa na kitu na Mungu akakitumia hicho kitu kupitishia Baraka zake uwe na uhakika hizo Baraka zitakuwa ni nyingi mno na kwa hiyo ni lazima uwe na vyombo vingi kwa ajili ya kukingia Baraka hizo! (amen?) nimesha kufundisha juu ya vyombo au kapu huko nyuma na ninaamini unaelewa ninaposema vyombo ninamaanisha nini!
Angalia mfano mwingine katika kitabu cha 2 Wafalme 7:3-6
“3 Basi walikuwapo watu wane wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, mbona tunakaa hapa hata tufe? 4 Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vilevile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu. 5 Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko,ili waende mpaka kituo cha washami; na walipofika mwanzo wa kituo cha Washami, kumbe! hapana mtu. 6 Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, tazama mfalme wa Israel amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi. 7 Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao,na punda zao, na kituo chao vilevile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao”.
Hiki ndicho kitu alichokiongelea ndugu Kimei akimuelezea baba askofu Laizer kwamba katika sifa ambayo yeye alipenda kwa baba askofu ni kile kitendo cha kuthubutu. Hii ni habari inayohusu mji wa Samaria amabao ulikuwa umezungukwa na majeshi ya Shamu(Syria) na hapakuwa na nafasi tena ya kufanya kazi ya kutafuta riziki wala shughuli zozote za kimaendeleo zilizofanyika! Hapa naomba nizungumze na ndugu zangu watanzania mnaosoma ujumbe huu, nazungumzia amani ya nchi yetu ambayo kuna daalili za watu wachache kwa maslahi yao binafsi wanataka kuivuruga amani hii amabayo Mungu ametujalia. Ndugu zangu hii amani tuliyo nayo kuna mataifa wanaitamani sana, kuna nchi ambazo kila kukicha wanapigana na tunaona wakimbizi wakikimbilia kwetu kwa sababu kuna amani. Hivyo ni wajibu wetu kulinda amani hii isitoweke maana ikitoweka mambo yatakuwa kama kwenye habari hii ninayokwenda kuielezea hapa chini. Sikiliza! Amani ikitoweka huo uhuru wa kuabudu ulionao hautaupata tena, amani ikitoweka huo uhuru wa kuamka asubuhi na kwenda kwenye shughuli za kujitafutia riziki hautaupata, hiyo nafasi ya kukaa kijiweni na rafiki zako hutaipata! Nafasi ya kwenda shule mwanafunzi hutaipata, nafasi ya kwenda saloon dada hutaipata! Nafasi ya kwenda shambani ewe mkulima hutaipata! Matokeo yake tutakuwa watumwa katika nchi yetu maana tutapoteza uhuru huu tulio nao. Inawezekana kwa bahati ujumbe huu umekufikia ndugu yangu muislam, hapo ulipo nakuomba kumbuka jinsi tulivyokuwa tukiishi pamoja na kwa amani tangu nchi yetu imepata uhuru, hebu tusiiruhusu hali yoyote ile itutenge na kutufanya maadui! Tusiruhusu kutumiwa na watu wachache wanaotaka kututumia ili kwa maslahi yao sisi tuuane na wao watuuzie silaha! Usikubali kutumiwa na mtu yeyote, mtumikie Mungu wako! Ndugu zangu nikirudi kwenye huo ujumbe hapo juu ni kwamba baada ya majeshi ya Shamu kuuzunguka mji wa Samaria ilifuata dhiki ambayo ilisababisha watu kukosa chakula hata kufikia kula nyama ya punda na biblia inasema hata kibaba cha mavi ya njiwa kikapata kuuzwa kwa vipande vitano vya fedha, sikiliza hapo sijakosea kuandika inasema kibaba cha mavi ya njiwa siyo nyama ya njiwa! Haikutosha ilifika wakati vyakula vilikosekana watu wakaanza kula watoto wao waliowazaa (inasikitisha sana!). tuombe Mungu tusijefikia mahali hapa. Katikati ya dhiki waliyokuwa nayo watu wa Samaria Mtu wa mungu Elisha akatangaza habari njema kwamba, “kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli,na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria. Sasa angalia hiyo mistari tuliyosoma hapo juu kuhusu wale watu wanne wenye ukoma, nilikwambia pale nyuma kuwa matatizo hayatatuliwi kwa wewe kuendelea kukaa kwenye tatizo na kulalamika juu ya hayo matatizo, bali matatizo yanatatuliwa kwa wewe kuamua kuchukua hatua ya kutatua tatizo. Ngoja nikwambie kitu hiki labda utanielewa, ni hivi Mungu anapenda watu wanaojaribu mambo!(wanaothubutu) Usichanganyikiwe!! Maana naona unajiuliza kivipi? Soma mistari hii ifuatayo utaelewa:- 28 Petro akamjibu akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.
29 Akasema njoo. Petro akashuka chomboni akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. 30 Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe………” (Mathayo 14:28-31)
Hii ni habari ya Bwana Yesu alipomaliza kufanya muujiza wa kulisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili na baada ya kumaliza aliwaamuru wanafunzi wake wapande mashuani watangulie kuvuka ng’ambo wakati yeye anaagana na watu. Baada ya kuagana na watu alikwenda mlimani kuomba na wakati huo wanafunzi wake walikuwa wameshafika katikati ya bahari. Biblia inasema wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea akienda kwa miguu juu ya bahari na wanafunzi walipomuona wakaogopa wakidhani wanaona kivuli (mzimu). Yesu akawaambia jipeni moyo ni mimi msiogope, na hapa sasa ndio tunakutana na maneno ya Petro akimwambia Yesu, Bwana IKIWA NI WEWE niamuru nije kwako juu ya maji!(huu ni ujasiri wa ajabu) Unajua kwa maneno mengine Petro alikuwa anasema Bwana mimi siamini kama ni wewe na nitaamini kuwa ni wewe pale utakaponiamuru nije kwako nikitembea juu ya maji! Wengine mkiambiwa kitu hata bila kupima mnakubali tu kwa sababu aliyesema ni mheshimiwa nabii au dk. Mchungaji na majina mengine mengi unayajua wanavyojiita. Sasa bila ya kupima unameza tu matokeo yake wengine wamejikuta wamemeza mawe! (pole sana). Sikiliza petro hakukubali kirahisi wale wanafunzi wengine walikubali kirahisi lakini yeye akasema ikiwa ni wewe…..! Bwana alimwambia petro njoo! Ninakwambia petro hakusubiri ushauri wowote ingawa hakuwahi kuona mtu anatembea juu ya maji hata siku moja haikumsumbua akashuka akaanza kutembea juu ya maji! Nilikwambia hapo nyuma kuwa ili uweze kutumiwa na Mungu ni lazima uwe na kitu ambacho kitamvuta Mungu kukusaidia au kukutumia na sasa nataka nikwambie kuwa mojawapo ya vitu vilivyofanya petro akafanywa kuwa jiwe (mwamba) ni hiki tulichokisoma hapa(kuthubutu). Kaangalie kwenye maandiko kama kulikuwa na mwanafunzi mdadisi na mwenye maswali mengi kama petro. Walipoulizwa wao wanamuona yesu kama nani wenzake walikaa kimya lakini yeye akasema wewe ni masihi mwana wa Mungu aliye hai! Mahali pengine aliwahi kumuuliza bwana sisi tumeacha vyote tukakufuata, tutapata nini? Wakati Yesu amekaa nao kwenye chakula cha mwisho aliwaambia juu ya mtu atakayemsaliti lakini Petro yeye alisimama akasema yeye yupo tayari kufungwa na hata kuuawa pamoja na Bwana na kama haitoshi ni yeye alimkata mtu sikio wakati yesu alipokuja kukamatwa! Kwa nini asifanywe mwamba? Ngoja nirudi kwenye somo letu, nimekwambia kuwa Mungu anapenda watu wanaojaribu mambo kwa hiyo ingawa Petro hakutembea sana kwenye maji kwa kuogopa kuzama lakini kitendo cha kuthubutu kuchukua hatua na kumwendea Bwana juu ya maji kilikuwa kitendo cha kijasiri ambacho wenzake hawakuthubutu kujaribu! Sasa ukirudi kwa wale wakoma wanne kama nilivyokwambia matatizo hayatatuliwi kwa mtu kuendelea kukaa kwenye hilo tatizo bali yanatatuliwa kwa mtu kuchukua(kuthubutu) hatua za kushughulika na hilo tatizo, wale jamaa wakaanza kuambiana,Mbona tunakaa hapa hata tufe? Wakasema tukikaa hapa tutakufa na tukisema tuingie mjini, mjini mna njaa huko nako tutakufa! Napenda sana jinsi hawa jamaa walivyojadiliana na ninataka nikwambie kitu wewe unaesoma ujumbe huu kwamba inawezekana plan A imekataa isikupe shida na kukukatisha tamaa tafuta plan B, wale jamaa wakasema ni bora tuakaliendee jeshi la washami kama wakituua na watuue lakini haiwezekani tukakaa hapa na kufa na njaa huku tunaona ,ooooh! Ninakwambia kumbe Mungu alikuwa anasubiri wafanye KWA UPANDE WAO kisha na yeye afanye kwa upande wake,alikuwa anasubiri wathubutu na ninakwambia wale jamaa walipoanza tu kuchukua(kuthubutu) hatua za kuondoka mahali pale (kwenye tatizo) biblia inasema, “Bwana aliwasikizisha washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa wakaanza kukimbia ili wajiponye nafsi zao”. (haleluyaaaaa!!) kumbe wakati wale wakoma wanatembea kuondoka zile hatua zao Mungu akazifanya zisikike kama kishindo cha jeshi kubwa kiasi majeshi ya adui yakaogopa na kukimbia!!( unaweza kumpigia bwana makofi hapo ulipo!). Wewe uliyekaa kwenye tatizo kwa muda mrefu na kubaki unalalmika Bwana amekuona na ameleta ujumbe huu kwako inuka kama walivyofanya wakoma wale wanne, chukua hatua kwa upande wako na Mungu atafanya kwa upande wake!!
Ni upande wa Yesu kumfufua Lazaro lakini kazi ya kuondoa jiwe na kumfungua sanda aende zake ni upande wetu sisi kufanya! KWASABABU MAMBO HAYAJILETI YENYEWE BALI YANASABABISHWA KUTOKEA!
Tafakari tunapomaliza kujifunza somo hili, BWANA na akuongeze zaidi unapoendelea kujifunza! Mungu akubariki kumbuka kuniombea ili niweze kutumika sawasawa na wito alioweka Mungu ndani yangu! Na usisahau kwamba, “50 Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni,kwamba mtu Akile asife”

–Mwal. Alfred T. Katuma.
+255786-996664
e-mail: alfredkatuma@yahoo.co.uk

Advertisements

About New Hope Ministry

Our ministry is based on Preaching the Gospel all over the world we preach the Gospel and we plant churches around the world. Contact us: Mobile: (255) 787589475 E-mail: newhopeministrytanzania@gmail.com
This entry was posted in HOME. Bookmark the permalink.

One Response to MAMBO HAYAJILETI YENYEWE – MAMBO YANASABABISHWA KUTOKEA!

  1. kone sailepu says:

    mwalimu bwana yesu apewe sifa nimebarikiwa sana nasomo lako na limenipa ujasiri sana mungu akubariki sana mtu wa mungu.

    Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s