Vurugu ugomvi wa Gas mtwara, Kikwete asema wanasiasa walihusika watakamatwa!

nyumba ikiwaka moto katika baadhi ya matukio ya vuruugu huko mtwara.

nyumba ikiwaka moto katika baadhi ya matukio ya vuruugu huko mtwara.

RAIS Jakaya Kiwete amesema serikali itawakamata wanasiasa wanaochochea vurugu mkoani Mtwara kwa kisingizio cha kuzuia gesi isitoke mkoani humo. Rais alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumzia vurugu kubwa zilizotokea Mtwara jana wakati akihutubia wananchi kwenye uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Dodoma – Iringa eneo la Bahiroad. Barabara hiyo ya kilomita 70 ni kutoka Dodoma mpaka Fufu.

Asubuhi alizindua Iringa-Mgole. Alisema kwamba gesi ya Mtwara ni rasilimali ya taifa na hakuna mtu anayeweza kusema kwamba ni mali yake.

“Tukisema zabibu ni ya Dodoma au kahawa ni ya Kilimanjaro tutakuwa tunatengeneza maajabu ya Mtwara… hatukubali… nchi hii ni moja na rasilimali zitumike kwa watu wote,” alisema Rais Kikwete.

Aidha alisema madai yanayotolewa na wachochea vurugu kuhusu rasilimali hiyo ya gesi hayakubaliki na hayana nafasi katika taifa la Tanzania. Rais alisisitiza katika hotuba yake kwamba rasilimali za nchi ni mali ya watu wote na watu wachache wasitafute umaarufu wa kisiasa kupitia gesi.

“Tutawakamata wanasiasa wote wanaochochea vurugu bila kujali mapembe yao.” Alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa Mtwara haijasahaulika katika matumizi ya rasilimali hiyo ya taifa. Alisema kuna mipango ya kutumia gesi kujenga viwanda vya mbolea na kutumia umeme kuunganisha gridi ya taifa kama ilivyo katika gesi ya Songosongo.

Alisema fujo za awali zilipoibuka kwa kisingizio cha kutotaka gesi itoke, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikwenda mkoani humo na wakaelezana, na alidhani kwamba walikuwa wameelewana lakini kumbe watu wenye chokochoko waliketi wakapanga mbinu wakisubiri bajeti ikisomwa waingie mtaani na kufanya fujo.

Alisisitiza kwamba taifa halitakubali kuacha kundi la watu wachache kuvuruga amani na kuwa serikali itawakamata wao na viongozi wao na kuwafikisha mahakamani.

Hali ilivyo Mtwara Wakati Rais Kikwete anatoa msimamo wake kuhusu ghasia hizo na hatua ambazo serikali yake itachukua, imeripotiwa kwamba watu kadhaa wakiwemo askari polisi wamekufa, huku nyumba, magari kuteketezwa na madaraja kubomolewa.

Hali hiyo tete iliyoukumba mji na hata baadhi ya vijiji vya mkoa huo, ilisababisha pia Bunge kuahirisha kikao chake cha jioni. Bunge jana jioni lilikuwa liendelee na mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyosomwa jana asubuhi.

Imedaiwa kwamba kiini cha vurugu hizo ni uchochezi unaoendeshwa kuupinga mpango wa Serikali wa kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam. Licha ya ujumbe wa Polisi Makao Makuu kwenda mkoani humo jana, Serikali inatarajiwa leo kutoa tamko bungeni, ikiwa ni pamoja na kuelezea hali halisi ya tukio hilo.

Waandishi wa habari Miongoni mwa walioathirika na vurugu hizo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho majengo yake sambamba na nyumba za viongozi wake wakiwemo madiwani zimechomwa.

Vile vile baadhi ya waandishi wa vyombo vya habari vya serikali na chama, wameathirika na vurugu hizo akiwemo Mwakilishi wa Televisheni ya Taifa (TBC), Kassim Mikongoro ambaye nyumba yake imechomwa.

Mwandishi wa gazeti hili, Hassan Simba na wa gazeti la Uhuru, pia walilazimika kukimbia nyumba zao baada ya kupewa taarifa kwamba kundi la wafanya vurugu walikuwa wakienda kuchoma nyumba zao.

Taarifa kutoka mkoani humo, zinasema kundi hilo lililokuwa likifanya vurugu, lilikuwa na silaha mbalimbali ikiwemo mabomu yanayotumika kuvulia samaki na wengine wanadaiwa kwamba walikuwa na magobori.

Katika eneo la Mikindani, ofisi zote za serikali zilivamiwa na kuchomwa moto. Aidha Daraja la Mikindani linatajwa kuwa limevunjwa kiasi kwamba ilikuwa vigumu kuingia wala kutoka mjini Mtwara. Kundi hilo la watu liliendelea hadi eneo la Shangani kwenye nyumba za viongozi.

Nyumba ya kupumzikia wageni inayoitwa Shengena Lodge ilichomwa moto kwa kile kinachoelezwa kwamba iliwapokea askari Polisi. Inadaiwa mmoja wa askari alichomwa mshale na watu hao.

Askari walifanya msako wa nyumba hadi nyumba maeneo ya Magomeni na Mangowela. Katika maeneo mbalimbali ya mji, milio ya risasi na mabomu ilitawala.

Matairi kila kona ya mji yalichomwa barabarani huku polisi na zimamoto wakifanya kazi ya kuzima huku ving’ora vikilia. Vurugu hizo ziliathiri pia watoto shuleni ambao walifungiwa huku walimu wakikimbia. Hakuna shughuli zozote zilizokuwa zikifanyika zaidi ya watu kujifungia majumbani kwa hofu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa hakupatikana mara moja kuelezea hali halisi ya vurugu hizo kutokana na hali ilivyokuwa tete.

“Kuna wananchi eneo la Mdenga wameonekana wakiwa na magobori. Baada ya kuvunja daraja la Mikindani, walianza kuelekea Kijiji cha Mpapu kwa lengo la kubomoa daraja lingine,” alisema mmoja wa watu walioshuhudia.

Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili, wamesema vurugu hizo ambazo zinadaiwa kufanywa na watu wanaopinga gesi kusafirishwa kutoka mkoani Mtwara, zinapaswa zichunguzwe kwa kina kubaini watu walio nyuma ya waandamanaji hao.

“Hapa utawaonea Polisi. Hizi ni vurugu za kisiasa ambazo haziwezi kumalizwa na nguvu ya dola. Wanasiasa wenyewe ndiyo wanapaswa kuzimaliza…wananchi hawawezi kujiunga bila kuwa na watu nyuma yao,” alisema mmoja wa watu ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mmoja wa askari kutoka mkoani Mtwara ambaye pia hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema “wanasiasa wanapaswa wabebe jukumu…unaweza ukalaumu polisi, lakini kama inaamua kufanya kazi ipasavyo, hawa hawa wanasiasa ndiyo hao hao utawaona wakiandamana kudai haki za binadamu.”

DCI atua Kwa mujibu wa tarifa kutoka Makao Makuu ya Polisi, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu ilimlazimu jana kwenda mkoani humo kwa ajili ya kudhibiti vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya saa sita.

Bunge laahirishwa Wakati hayo yakiripotiwa kutokea Mtwara, kikao cha Bunge kilichotarajiwa kuendelea jana jioni mjini Dodoma ili kujadili hotuba hiyo ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kiliahirishwa na Spika wa Bunge Anne Makinda.

Mara baada ya kuingia kwenye ukumbi wa Bunge, Spika wa Makinda aliwatangazia wabunge kwamba kikao hicho kisingeweza kufanyika kutokana na vurugu zilizotokea mkoani Mtwara.

“Waheshimiwa wabunge hotuba hii ya wizara ya nishati na madini ilipaswa kujadiliwa kwa siku mbili lakini hata kabla ya nusu siku kufika, tulipata taarifa kwamba kungetokea machafuko Mtwara. Hivyo basi, naiagiza Serikali kulifuatilia suala hili ili kesho itoe taarifa rasmi ya hali halisi ilivyo na muda huu, kamati ya uongozi ya Bunge itakutana ili kujadili suala hilo, hivyo naahirisha kikao hiki cha bunge hadi saa tatu asubuhi kesho.”

Magari yakwama Lindi Abiria zaidi ya 455 wamekwama katika kituo cha mabasi mjini Lindi mkoani humo kutokana na vurugu hizo za Mtwara anaripoti Keneddy Kisula.

Dereva wa basi la abiria la Maning Nice linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, Rashid Ahmad alisema kwamba kuna wasi wasi wa usalama wa abiria, mali zao na magari yao kuharibiwa.

Taarifa zilizopatikana mjini Lindi, zilisema magari kadhaa yalichomwa moto. Inadaiwa katika Kijiji cha Madangwa, gari ndogo aina ya Suzuki Vitara liliunguzwa kwa moto.

Licha ya wenye magari kugoma kuondoka Lindi kwenda Mtwara, pia abiria waliridhia na kuamua kubaki mjini hapa hadi wahakikishe usalama umeimarika.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga alisema jeshi hilo liko tayari kuwasindikiza mpaka mwisho wa safari yao. Alisema kwamba serikali iko tayari kutoa msaada wa ulinzi kwa mabasi hayo yenye abiria yapatayo saba yaliyokwama. Mabasi hayo ni Maning Nice, Shilingi, Hamanju, No Rise, Buti la Zungu, Ng’itu na Machinga.

Advertisements

About New Hope Ministry

Our ministry is based on Preaching the Gospel all over the world we preach the Gospel and we plant churches around the world. Contact us: Mobile: (255) 787589475 E-mail: newhopeministrytanzania@gmail.com
This entry was posted in HOME. Bookmark the permalink.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s